Skip to main content




UANDISHI


UANDISHI WA INSHA ZA KIADA


Insha ni kifungu cha maandishi kilichoandikwa kutokana na mtazamo wa mwandishi katika kujadili juu ya mada fulani. Mwandishi anaweza kuandika kuipinga mada hiyo au kuishadidia mada hiyo. Kuna aina mbili za insha, insha za kaida (zisizo za kisanaa) na insha za kisanaa.


Insha za kaida ni insha zinazotumia lugha ya kawaida kuelezea mambo mbalimbali katika jamii, mfano juu ya mazingira, uchumi, biashara, historia n.k.




Muundo wa Insha za Kaida


Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo:


1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k


2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako.


3. Kiini cha insha; katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo haya yanakuwa katika aya kadhaa kulingana na idadi ya hoja ulizonazo katika mjadala wako.


4. Hitimisho; hapa ndipo kuna muhtasari wa kile kilichojadiliwa katika kiini cha insha au inaweza kuwa ni msimamo juu ya kile kilichohadiliwa katika insha.




Mambo ya Kuzingatia katika Uandishi wa Insha


Taratibu za uandishi zinapozingatiwa insha pia itasomeka vizuri na pia itakuwa na mtiririko mzuri wa mawazo.


1. Epuka kutumia vifupisho vya maneno visivyo rasmi.
Uandishi wa insha ni suala rasmi, kwa hiyo katika uandishi wake inatakiwa kuzingatia kuepuka kutumia vifupisho ambavyo sio majumui yaani havijulikani. Kwa mfano maandishi kama, xamahani (samahani), ckatai (sikatai) na mengine yafananayo kama hayo ni lazima yaepukwe katika uandishi wa insha.


2. Andika utangulizi unaovuta umakini wa msomaji.
Hiki ni kipangele cha muhimu sana, msomaji anapoona kwamba kwenye utangulizi hakuna kitu kinachomvutia hataendelea kuhangaika kusoma insha hiyo.


3. Andika kiini cha insha kwa mpangilio mzuri.
Unatakiwa kuandika insha yako katika mpangilio mzuri huku kila wazo kuu likipewa aya yake na kuwepo na mtiririko mzuri wa mawazo.


4. Andika hitimisho la insha likiwa linahitimisha mawazo yaliyokwishajadiliwa katika kiini. Hakikisha unapofanya hitimisho epuka kudokeza wazo jipya ambalo linazua mjadala mpya, hakikisha hitimisho lako linabeba mawazo uliyokwisha yajadili katika insha yako na wala yasiwe mawazo yanayotoka nje ya kile ulichokijadili.





UANDISHI WA HOTUBA


Hotuba ni insha ambayo hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/kiongozi anapozungumzia hadhira, kuhusu jambo fulani. Insha ya hotuba huandikwa katika hali ya usemi halisi na mwandishi hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza insha yake. Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi, shirika fulani, daktari, n.k. Hadhira katika hotuba husheheni wageni waalikwa, wanachama, wafuasi, wananchi, n.k ambao wanahusishwa katika mada inayorejelewa katika hotuba hiyo.




Muundo wa Hotuba


Hutuba inakuwa na muundo ufuatao:
Anwani
Anwani, mada au kichwa cha hotuba hurejelea mada ya hotuba. Pia mada inaweza kutaja hadhira.
Hotuba ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya ukimwi kwa wananchi.
Hotuba ya Mwalimu Mkuu kwa Wazazi
Utangulizi
Anza hotuba yako kwa kuwatambua waliohudhuria mkutano (hadhira).
Wataje kwa majina/vyeo vyao kuanzia yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na mabwana. Kumbuka kwamba hauhitajiki kuwasalimia. Kuwatambua kwa majina pekee kunatosha.
Jitambulishe kwa hadhira yako hasa ikiwa unazungumzia hadhira isiyokujua au wageni.
Tanguliza mada yako.

Kwa mfano:
Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya, Mhe. Mbunge, wanachama wa kikundi hiki cha Mazingira, mabibi na mabwana. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu buheri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa Kikundi cha Mazingira na jioni ya leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote tulifahamu ili kuboresha mazingira yetu kwa …


Kiini
Hakikisha kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi mwisho
Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisia wala si wa taarifa.
Tamati
Hakikisha kwamba mwisho wa hotuba yako unatambulika.
Unaweza kumaliza kwa shukurani





UANDISHI WA RISALA


Risala ni hotuba fupi inayosomwa mbele ya kiongozi kwa niaba ya kundi fulani la watu hasa hasa wanafunzi, wafanyakazi, washiriki, wanachama, mafundi n.k ili kutoa maelezo ya haja zao mbalimbali na mahitaji yao au kuonyesha msimamo wa kundi hilo kwa kiongozi.



Muundo wa Risala


Utanguizi
Cheo cha kiongozi anayehusika
Kundi linalowakilishwa
Kiini
Maelezo ya hali halisi ya maswala na msimamo wa kundi linalowakilishwa.
Mapendekezso na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa.
Hitimisho
Shukrani
Tanbihi: Kama vilivyosemwa awali risala ni hotuba fupi lakini inachukua mambo muhimu tu na kuyaeleza. Hivyo risala yenyewe huwa ni maelezo ya muhtasari kwa jambo linalohitaji maelezo marefu Katika hotuba. Utungaji wa risala unahitaji uangalifu sana na lugha ya heshima iliyo wazi kueleweka kwa kiongozi.



Mfano wa Risala:


Ndugu Mgeni rasmi, Walimu, Wanafunzi wenzetu, Wazazi, Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.


Kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha nne, tunayo heshima na furaha kubwa , kukukaribisha ili ushiriki nasi katika siku hii muhimu na kusikia mafanikio mbalimbali kwa kipindi chote cha masomo yetu hapa shuleni.


Shukrani zetu za pekee na za dhati ziende kwa uongozi mzima wa Shule na walimu wetu wote kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa kutufundisha, hivyo tumefundishika vyema; kwasababu tupo tofauti sana na tulivyokuja hapa mwezi januari 2009.


Ndugu mgeni rasmi, tulianza kidato cha kwanza tukiwa wanafunzi 120; wasichana 60 na wavulana 60. Mpaka leo tunapohitimu tupo wanafunzi 90; kati yao wavulana ni 43, na wasichana 47. Wengine wameshindwa kuhitimu nasi siku ya leo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ujauzito na kuhama shule. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema wa Baraka kwa ulinzi wake kwetu hadi leo hii tunahitimu kidato cha nne.


Ndugu mgeni rasmi, elimu hii ya kidato cha nne imetupatia msingi mzuri wa kujiunga na Elimu ya juu, pia imetujengea uwezo mzuri wa kujitambua na kufikiri, kufanya kazi vizuri na kufanya maamuzi sahihi; pia imetuwezesha sisi wanafunzi kupata elimu ya mambo mbalimbali kupitia masomo tunayo fundishwa hapa shuleni, mfano; tumepata elimu ya uraia, historia ya mambo mbalimbali katika nchi yetu na dunia kwa ujumla, pia tumeweza kupata uelewa kuhusu afya na magonjwa, usalama katika mazingira yetu, Kilimo, Maumbile ya nchi, hali ya hewa, misitu, na viwanda. Vilevile tumeelewa umuhimu wa kusoma vitabu mbalimbali kwa lengo la kupata ujuzi wa kuinua uchumi wetu wa taifa.


Ndugu mgeni rasmi, mafanikio hayo yamepatikana kwasababu ya ushirikiano mzuri kati yetu na walimu wetu. Tangu tujiunge na shule hii tukiwa kidato cha kwanza tumefanya majaribio na mitihani ya mara kwa mara jambo lililo tusaidia kuinua taaluma yetu.Tunawashukuru sana walimu wetu, tuna waahidi kufanya vizuri katika mitihani yetu ya Taifa ya kidato cha nne mwaka huu, na Mungu awabariki sana.


Ndugu mgeni rasmi, tumepata changamoto mbalimbali wakati wa maisha yetu ya kielimu hapa shuleni, kama ifuatavyo;


Ndugu mgeni rasmi, tuna changamoto ya upungufu wa vitabu vya kiada na ziada; hii imepelekea kushindwa kujisomea vizuri, kwani kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya ishirini (20).


Ndugu mgeni rasmi, changamoto nyingine ni upungufu wa vifaa vya maabara, hii inapelekea kuchangia kifaa kimoja, hivyo tuna tumia muda mwingi sana kujifunza na kumuelewa mwalimu.


Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa walimu, hasa wa masomo ya sayansi; hii imepelekea kutomaliza ‘syllabus’ kwa wakati.


Ndugu mgeni rasmi, pia kuna changamoto ya upungufu wa samani za shule, kama vile; madawati kwa ajili ya wanafunzi, viti na meza kwa ajili ya walimu; hii imepelekea baadhi ya wanafunzi wenzetu kukaa wawili kwenye dawati moja.


Ndugu mgeni rasmi, maji ni changamoto hapa shuleni, kwani shule haina kisima cha maji, hii imepelekea shule kununua maji kwa gharama kubwa, ambayo hayatoshelezi mahitaji ya shule, kama vile usafi; hususani kwa upande wa vyoo, bila kuwa na maji ya kutosha tutapata magonjwa ya mlipuko, kama vile kipindupindu.


Ndugu mgeni rasmi, changamoto ya vifaa vya michezo; kama unavyojua kuwa michezo ni afya, shule yetu ina upungufu mkubwa wa vifaa vya michezo kama vile; mipira ya miguu, pete na mikono, pia hatuna milingoti ya chuma kwaajili ya magoli ya viwanja vya michezo yote tunayocheza hapa shuleni.


Ndugu mgeni rasmi, tunashukuru uongozi wa shule hii, walimu na wazazi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya shule yetu; kwa upande wa masomo ya sayansi; shule imeweza kutenga chumba kimoja cha darasa kitumike kama maabara japo kuwa kuna upungufu mkubwa wa vifaa.


Ndugu mgeni rasmi, tunayo matumaini kwamba maombi yetu umeyasikiliza na utayaatekeleza, maana tunajua kwamba wewe unaweza kupitia Hlimashauri unayo isimamia, asante sana.


Mwisho tunaomba msamaha wa dhati toka moyoni mwetu kwa Walimu, Wanafunzi wenzetu na Wazazi pale tulipoenda kinyume na matazamio yenu, kwani watu wakiishi pamoja tofauti lazima ziwepo, tunatumaini mtapokea msamaha wetu, nasi hatuna jambo lolote baya kwenu.


Ndugu mgeni rasmi, tuna kushukuru sana kwa kufika katika Mahafali yetu, kwani tunatambua kuwa unamajukumu mengi ambayo umeyaacha na kuwepo hapa kwaajili yetu.






UANDISHI WA KUMBUKUMBU ZA MIKUTANO


Kumbukumbu za mikutano ni rekodi zinazowekwa na katibu wa mkutano wakati mkutano unapoendelea ili kuhifadhi yanayojadiliwa na kukubaliana katika mkutano huo. Katibu anapaswa kufuatilia mtindo maalum wa kuandika kumbukumbu hizo kulingana na mpangilio katika mkutano.




Mambo ya Kuzingatia katika Uchukuaji wa Kumbukumbu za Mikutano



Mambo ya kuzingatia katika uandishi wa kumbukumbu ni kama yafuatayo:


1. Kichwa cha kumbukumbu – Kichwa cha kumbukumbu kinapaswa kutaja mambo yafuatayo: Ni mkutano wa akina nani? Unaandaliwa wapi? Unaandaliwa lini? Unaanza saa ngapi? Mfano wa Kichwa cha Kumbukumbu: Kumbukumbu za Mkutano wa Shirika la Msalaba Mwekundu Shuleni ulioandaliwa tarehe saba Agosti 2001 katika Ukumbi wa Mikutano kuanzia saa Tisa alasiri.


2. Waliohudhuria – Andika orodha ya wote waliofika kwenye mkutano huku kuanzia na yule mwenye cheo cha juu zaidi hadi kwa wanachama. Pia onyesha vyeo vyao.


3. Waliotoa Udhuru -Hawa ni wale walioomba ruhusa kutohudhuria mkutano


4. Waliokosa kuhudhuria - Hawa ni waliokosa kuhudhuria mkutano, bila kutoa udhuru)


5. Waalikwa - Hawa ni wageni walioalikwa katika mkutano, k.v mlezi wa chama, afisa wa kiutawala, n.k)

6. Ajenda -orodhesha hoja zitakazorejelewa katika mkutano huo




Kumbukumbu



KUMB 1
Kumbukumbu ya kwanza huwa ni kufunguliwa kwa mkutano na ujumbe kutoka kwa mwenyekiti.

KUMB 2
Kusomwa kwa kumbukumbu za mkutano uliotangulia na kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo kwa kutiwa saini.

KUMB 3
Maswala yanayoibuka kutokana na kumbu kumbu zilizosomwa. (Kumbuka kutaja nambari ya kumbu kumbu hizo)

KUMB kuendelea
Maswala katika ajenda

KUMB ya Mwisho
Maswala mengineyo yasiyokuwa kwenye orodha ya ajenda.

Tamati
Kufungwa kwa mkutano. Taja mkutano ulifungwa saa ngapi; mkutano ujao utakuwa tarehe ngapi; kisha acha nafasi ya kuthibitishwa kwa kumbu kumbu hizo katika mkutano utakaofuatia.



Mfano:
KUMBUKUMBU ZA MKUTANO WA CHAMA CHA KISWAHILI ULIOANDALIWA KATIKA CHUMBA CHA MIJADALA TAREHE 24 JUNE 2013 KUANZIA SAA TATU ASUBUHI


Waliohudhuria
Teddy Mbogela – Mwenyekiti
Vaileth Matiko – Mweka hazina
Iliashibu Masatu – Mkuu wa utafiti
Funk Kiduku – mwanachama
Meta Mkorofi – katibu
Waliotuma Udhuru
Bahatika Mashauri – Naibu Mwenyekiti
Ponea Kamgazi – Msimamizi wa Mijadala
Waliokosa Kuhudhuria
Zebedayo Chisege – Spika
John Kumbikumbi – mwanachama
Waalikwa
Mnoko Nokwe – Mwanahabari
Dkt. Fikirini– Mlezi wa Chama.
Ajenda
Uchapishaji wa jarida la Kiswahili
Shindano la kuandika insha.
Kusajili wanachama wapya

KUMBUKUMBU 3/04/14 – KUFUNGULIWA KWA MKUTANO
Mwenyekiti aliwakaribisha wanachama wote na baada ya kuwatambulisha wageni, akawaomba washiriki wawe huru kuchangia katika ajenda mkutano huu ili kuboresha chama.


KUMBUKUMBU 7/04/14 – KUREJELEA KUMBUKUMBU ZA MKUTANO ULIOPITA
Katibu alisoma kumbukumbu za mkutano wa mwezi Machi. Kumbukumbu zilikubaliwa na wanachama wote na kuthibitishwa na mwenyekiti pamoja na katibu kwa kutia saini.


KUMBUKUMBU 10/04/14 – MASWALA IBUKA KUTOKANA NA KUMBUKUMBU ZILIZOSOMWA
Mweka hazina alifahamisha mkutano kwamba aliongea na mkuu wa idara ya Kiswahili kuhusu ufadhili kama tulivyokuwa tumekubaliana katika KUMB 9/03/10 ya mkutano uliopita.


KUMBUKUMBU 12/04/14 – HAFLA YA KISWAHILI
Iliripotiwa kwamba hafla ya Kiswahili ambayo wanachama walikuwa wamealikwa kuhudhuria katika Shule ya Sakata Academy haingeweza kufanyika kutokana na tamasha la muziki lilizokuwa linaendelea katika shule hiyo. Wanachama waliokuwa wamejitayarisha kwa mashairi waliombwa kuendelea kujifunza ili wayawasilishe muhula wa pili.


KUMBUKUMBU 15/04/14 – UCHAPISHAJI WA JARIDA LA KISWAHILI
Wanachama walikubaliana:
Kwamba chama kitaanza kuchapisha jarida la Kiswahili
Kwamba jarida litakuwa likichapishwa mara moja kila muhula na kuuzwa shuleni
Kwamba kila mwanachama atachangia katika kuandika makala na kuuza nakala za jarida hilo.
Kwamba paneli ya wahariri lingeundwa ili kuongoza idara ya uchapishaji
Kwamba hazina ya chama ina fedha za kutosha kuzindua uchapishaji huo.


KUMBUKUMBU 17/04/14 – SHINDANO LA KUANDIKA INSHA
Kila muhula wa pili, chama huandaa shindano la kuandika insha ambalo wanafunzi wote hushiriki. Insha zilizopendekezwa mwaka huu ni:
“Jadili chanzo cha migomo shuleni na namna ya kusuluhisha.”
… … … … … … … … …
… … … … … … … … …
… … … … … … … … …


KUFUNGWA KWA MKUTANO
Mkutano ulifungwa saa kumi na nusu, baada ya maswala yote kujadiliwa. Mkutano unaofuatia ulipoangwa kuwa tarehe ishirini mwezi Mei, katika Ukumbi wa Muziki.


KUTHIBITISHWA KWA KUMBUKUMBU


______________
_____________

Mwenyekiti
Katibu



Tarehe:________
Tarehe:________




Popular posts from this blog

UFAHAMU UFAHAMU WA KUSIKILIZA Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe. Kujibu Maswali ya Habari Uliyosikiliza Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha: Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa. Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo: 1. Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema. 2. Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji an...
UENEAJI WA KISWAHILI ENZI ZA WAINGEREZA NA BAADA YA UHURU Ukuaji na Ueneaji wa Kiswahili katika enzi ya Waingereza Waingereza walipochukua koloni la Tanganyika kutoka kwa Wajerumani walikuta Kiswahili kimeimarika na kinatumika katika maeneo mengi ya nchi. Kwa kuwa nao walihitaji kutawala hawakupuuzia matumizi ya Kiswahili katika utawala wao japo hawakutumia Kiswahili kwa lengo la kukikuza lakini walijikuta wanakieneza na kukikuza bila ya wao kukusudia. Mambo waliyochangia Waingereza katika Ukuaji wa Kiswahili nchini Tanzania Waingereza walitumia Kiswahili kama nyenzo ya kusaidia shughuli zao za kiutawala. Hata hivyo kuna mambo waliyofanya waingereza yaliyosaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili, mambo hayo ni kama yafuatayo: 1. Shuguli za Kiuchumi Shuguli za kiuchumi wakati wa Waingereza zilihusisha kilimo na biashara. Kwa upande wa klimo, Waingereza waliendesha kilimo cha mazao mbalimbali, na walitumia mfumo wa kuajiri vibarua kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Vibarua h...
KUTUNGA KAZI ZA FASIHI ANDISHI UTUNGAJI WA MASHAIRI Utungaji/uandishi wa kubuni ni ule unatokana na hisia ambazo zinamsukuma mtunzi ili atunge kazi yake. Hisia zinaungana na wazo ambapo vitu hivyo vinamsumbua akilini na kumkosesha raha. Mwandishi wa kubuni anataka aliwasilishe wazo lake ili hadhira ifahamu kilichopo moyoni mwake. Mwandishi hukosa usingizi na hivyo hulazimika kuamka na kuandika kile kinachomsukuma akilini mwake. Mambo ya Kuzingatia katika Utungaji wa Mashairi Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja. 1. Kuona: je, mhusika unayemfikiria kichwani mwako unamwonaje? Umbo lake ni la kuvutia au kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya golori au la? Ni makubwa au madogo? Je, ni mlemavu wa macho? 2. Kunusa: pua zako zinakufanya usikie harufu gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je, ni uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka...
KUONGEZA MSAMIATI WA KISWAHILI Uundaji wa Maneno Lugha hukua na kubadilika kila wakati kulingana na maendeleo ya jamii. Kigezo kimojawapo cha kukua na kubadilika kwa lugha ni kuongezeka kwa msamiati. Ili msamiati uongezeke katika lugha sharti maneno mapya yaundwe. Njia za Uundaji Maneno Uundaji wa Msamiati hutokea kwa njia mbalimbali zifuatazo: Kubadili mpangilio wa herufi. Kuambatanisha maneno. Kutohoa maneno ya lugha nyingine. Uambishaji wa maneno. Kufanikisha sauti, umbo, mlio na sura. Kuunda Msamiati kwa kubadili Mpangilio wa Herufi Neno hujengwa kwa vitamkwa au herufi. Neno jipya lenye maana tofauti huweza kuundwa kwa kubadili mpangilio wa neno lingine Mfano Neno lima, lina herufi l, i, m, a, herufi hizi huweza kujenga maneno kama mali, kumi,imla, mila. Neno tua lina herufi t, u, a, herufi hizi zina weza kujenga maneno kama:- tatu, tua, viatu, tatua. NJIA YA KUAMBATANISHA MANENO Kuna njia tatu za kuambatanisha meneno Njia ya kurudufisha au kukariri neno M...