Skip to main content




KUTUNGA KAZI ZA FASIHI ANDISHI


UTUNGAJI WA MASHAIRI


Utungaji/uandishi wa kubuni ni ule unatokana na hisia ambazo zinamsukuma mtunzi ili atunge kazi yake. Hisia zinaungana na wazo ambapo vitu hivyo vinamsumbua akilini na kumkosesha raha. Mwandishi wa kubuni anataka aliwasilishe wazo lake ili hadhira ifahamu kilichopo moyoni mwake. Mwandishi hukosa usingizi na hivyo hulazimika kuamka na kuandika kile kinachomsukuma akilini mwake.




Mambo ya Kuzingatia katika Utungaji wa Mashairi


Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja.


1. Kuona: je, mhusika unayemfikiria kichwani mwako unamwonaje? Umbo lake ni la kuvutia au kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya golori au la? Ni makubwa au madogo? Je, ni mlemavu wa macho?


2. Kunusa: pua zako zinakufanya usikie harufu gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je, ni uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka kikwapa au uturi? Je, ananuka mdomo?


3. Kuhisi: je, unapokaa karibu naye unajihisi nini? Je, unapata mhemko wowote au huhisi chochote? Je, akikupapasa mwilini mwako unajisikia nini? Akikugusa bega unajisikia nini?


4. Kuonja: je, ukiweka kitu hicho mdomoni unaonjaje – ni chungu au tamu? Je, ina pilipili au masala? Je, kuna chumvi au sukari? Je, kitu hicho kina ukakasi au uchachu?


5. Kusikia: je, sauti unayoisikia ikoje? Inamtoa nyoka pangoni? Inakufanya ukose usingizi? Je, ni sauti nzuri au mbaya? Ni nyororo au nzito? Kama ni sauti ya muziki – je, iko chini au juu (kelele)?



Uzoefu wa Mwandishi


Uzoefu ni hali ya kukaa au kujishughulisha na jambo au kitu kwa muda mrefu. Mwandishi ana uzoefu (uzoevu) wa kukabiliana na maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani ambayo umekutana nayo katika maisha yako? Je, ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011) kuna baadhi ya watu waliokolewa na magodoro ya Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama yasingekuwa na nailoni? Uzoevu/uzoefu wako ukoje?




Uchunguzi/utafiti


Uchunguzi unapaswa ufanywe na mwandishi ili aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa kufanya udanganyifu, mwandishi atapoteza imani yake kwa wasomaji wa kazi zake. Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu, mnyama, mdudu na kadhalika – anatembeaje, anakulaje, analalaje, anaishije, anachekaje, analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na mazingira yake? Haya ni maswali muhimu katika kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue kitu anachotaka kukiandika akiandikaje na akiwasilishaje ili aweze kuikamata hadhira yake.


Mwandshi baada ya kuzingatia mambo haya sasa anaweza kuanza kutunga kazi yake. Hapa sisi tutajikita zaidi katika utunzi wa mashairi. Kabala hatujaenda katika hatua ya utunzi ni muhimu kujua dhana ya shairi kwa ujumla wake, na baada ya hapo tutakuwa tumekwisha pata maarifa yakutosha juu ya mashairi ambayo yatatuwezesha kutunga mashairi.





DHANA YA SHAIRI


Shairi ni kipande cha maandishi kilichopangwa kwa utaratibu katika mistari. Sauti za silabi hufanana zikiwa kati au mwisho mwa mstari. Maandishi hayo yakisomwa huleta ujumbe na hisia fulani ya kimaisha.


Mpango wa maneno ya shairi, ambao huweza kuimbwa hutoa picha wazi, maana halisi na burudani ya kimuziki. Nyimbo nyingi za makabila zimepangiliwa kishairi ijapokuwa hazikuandikwa


Mashairi yana umbo ambalo huonekana kwa mpangilio wa sauti na idadi ya maneno katika mistari. Umbo hili hutofautisha shairi na tenzi. Kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufahamika kuhusu shairi, nayo ni:


1. Beti – Kifungu kimoja cha shairi ambacho kina uzani sawa.


2. Vina – Ni mwisho wa mistari ambayo huwa na silabi zenye sauti ileile mwishoni mwa sentensi.


3. Mizani – Ni idadi zilizo sawa za silabi katika kila mstari, ubeti hadi ubeti.


4. Kituo – Huu ni mstari wa mwisho wa ubeti. Kuna vituo vya aina tatu:Kituo cha bahari – ni mstari unaotoka mwanzo hadi mwisho bila kubadilika katika kila ubeti;Kituo cha kimalizio – ni kituo ambacho mstari wa mwisho maneno yake hubadilika ubeti hadi ubeti;Kituo nusu bahari – ni mstari wa mwisho ambao maneno yake nusu hubadilika na nusu hubaki kama ulivyo ubeti hadi ubeti.


Katika mashairi (ya kimapokeo), kila mstari lazima uwe umekamilika na ubeti uwe na maana kamili.


Vipengele vya Fani katika Mashairi
Jina / anwani
Mandhari
Wahusika
Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa, sabilia n.k
Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana vina, kurudiwa kipande kizima cha mstari wa mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti unaofuatia.


Vipengele vya Maudhui katika Mashairi
Vipengele vya maudhui ni pamoja na: migogoro, ujumbe, falsafa, msimamo, mtazamo, na dhamira za mwandishi.
Matumizi ya ushairi ni pamoja na: kuomboleza, kubembeleza, kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na kadharika.
Baada ya hapa sasa unaweza kuanza kutunga shairi lako la kwanza.

Popular posts from this blog

UFAHAMU UFAHAMU WA KUSIKILIZA Ufahamu wa kusikiliza ni zaidi ya kusikiliza tu kile kilichosemwa; badala yake ni uwezo wa mtu kuelewa maana ya maneno anayoyasikia na kuweza kuhusiana nayo kwa namna fulani. Kwa mfano mwanafunzi anaposikiliza hadithi, ufahamu mzuri wa kusikiliza humsaidia kuielewa hadithi hiyo, kuikumbuka, kuijadili, na hata kuisimulia tena kwa maneno yake mwenyewe. Kujibu Maswali ya Habari Uliyosikiliza Ufahamu wa kusikiliza unahusisha michakato kadhaa katika kuelewa na kupata maana ya kile kinachozungumzwa. Michakato hii inahusisha: Kuelewa vizuri sarufi ya lugha ile inayozungumzwa Kuelewa vyema maana ya maneno ya mhusiaka anayezungumza Kuelewa sintaksia (muundo wa maneno) ya sentensi kwa namna zinavyowasilishwa. Katika ufahamu wa kusikiliza, msikilizaji hana budi kuzingatia mambo yafutayo: 1. Kuwa makini na kuelekeza akili yote kwa mzungumzaji ili kuweza kusikia kila anachokisema. 2. Kutilia maanani vidokezo vya maana ili kubaini iwapo msemaji an...
UENEAJI WA KISWAHILI ENZI ZA WAINGEREZA NA BAADA YA UHURU Ukuaji na Ueneaji wa Kiswahili katika enzi ya Waingereza Waingereza walipochukua koloni la Tanganyika kutoka kwa Wajerumani walikuta Kiswahili kimeimarika na kinatumika katika maeneo mengi ya nchi. Kwa kuwa nao walihitaji kutawala hawakupuuzia matumizi ya Kiswahili katika utawala wao japo hawakutumia Kiswahili kwa lengo la kukikuza lakini walijikuta wanakieneza na kukikuza bila ya wao kukusudia. Mambo waliyochangia Waingereza katika Ukuaji wa Kiswahili nchini Tanzania Waingereza walitumia Kiswahili kama nyenzo ya kusaidia shughuli zao za kiutawala. Hata hivyo kuna mambo waliyofanya waingereza yaliyosaidia kukua na kuenea kwa Kiswahili, mambo hayo ni kama yafuatayo: 1. Shuguli za Kiuchumi Shuguli za kiuchumi wakati wa Waingereza zilihusisha kilimo na biashara. Kwa upande wa klimo, Waingereza waliendesha kilimo cha mazao mbalimbali, na walitumia mfumo wa kuajiri vibarua kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Vibarua h...
UANDISHI UANDISHI WA INSHA ZA KIADA Insha ni kifungu cha maandishi kilichoandikwa kutokana na mtazamo wa mwandishi katika kujadili juu ya mada fulani. Mwandishi anaweza kuandika kuipinga mada hiyo au kuishadidia mada hiyo. Kuna aina mbili za insha, insha za kaida (zisizo za kisanaa) na insha za kisanaa. Insha za kaida ni insha zinazotumia lugha ya kawaida kuelezea mambo mbalimbali katika jamii, mfano juu ya mazingira, uchumi, biashara, historia n.k. Muundo wa Insha za Kaida Katika uandishi wa insha, muundo wake unakuwa na vitu vifuatavyo: 1. Kichwa cha insha; kichwa cha insha hudokeza kile ulichokijadili katika insha yako. Kwa mfano: Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya n.k 2. Utangulizi; Mambo yaliyopo katika utangulizi ni pamoja na kutoa fasili ya maneno muhimu na kuelezea kwa muhtasari mambo ambayo utakwenda kuyajadili katika insha yako. 3. Kiini cha insha; katika kiini ndipo kuna maelezo ya kina juu ya kile unachokijadili katika insha yako, maelezo ...
KUONGEZA MSAMIATI WA KISWAHILI Uundaji wa Maneno Lugha hukua na kubadilika kila wakati kulingana na maendeleo ya jamii. Kigezo kimojawapo cha kukua na kubadilika kwa lugha ni kuongezeka kwa msamiati. Ili msamiati uongezeke katika lugha sharti maneno mapya yaundwe. Njia za Uundaji Maneno Uundaji wa Msamiati hutokea kwa njia mbalimbali zifuatazo: Kubadili mpangilio wa herufi. Kuambatanisha maneno. Kutohoa maneno ya lugha nyingine. Uambishaji wa maneno. Kufanikisha sauti, umbo, mlio na sura. Kuunda Msamiati kwa kubadili Mpangilio wa Herufi Neno hujengwa kwa vitamkwa au herufi. Neno jipya lenye maana tofauti huweza kuundwa kwa kubadili mpangilio wa neno lingine Mfano Neno lima, lina herufi l, i, m, a, herufi hizi huweza kujenga maneno kama mali, kumi,imla, mila. Neno tua lina herufi t, u, a, herufi hizi zina weza kujenga maneno kama:- tatu, tua, viatu, tatua. NJIA YA KUAMBATANISHA MANENO Kuna njia tatu za kuambatanisha meneno Njia ya kurudufisha au kukariri neno M...